Stori: Waandishi WetuHABARI ya mjini hivi sasa ni kuhusu bifu linalotembea chini kwa chini kati ya nyota wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anadaiwa kumchefua vilivyo dada yake wa hiyari, Rose Alphonce Nungu ‘Muna’.
Muna ni kati ya watu muhimu waliomsaidia Lulu tangu akiwa nyuma ya nondo, katika Gereza la Segerea baada ya kuwekwa mahabusu wakati akisubiria shauri lake la kesi ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba inayomkabili.ISHU KAMILI
Habari za moto kutoka kwa chanzo chetu cha kuaminika, zinasema kuwa Muna amewaka sana kutokana na kitendo cha Lulu kumtenga katika shughuli yake ya Kibao Kata iliyofanyika wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Letasi Lounge, Victoria, Dar.
SOSI ANATIRIRIKA
Kwa sharti la kutochorwa jina lake gazetini, sosi huyo ambaye ni shosti wa karibu na Muna na Lulu, alisema kisa kilianzia pale ambapo Lulu aliahidi ahadi ambazo hakuzitimiza na kumuacha mwenzake kwenye mataa.
“Lulu hajamfanyia mwenzake kitu kizuri, hata hivi Muna anavyolalamika ni haki kabisa. Ujue alimuahidi vitu vingi kwenye shughuli yake, Muna na wajumbe wengine wakamtegemea, mwishowe akamkimbia.
“Hata kama ungekuwa wewe lazima ingekuuma, mtu umsaidie vile... umjali kama ndugu yako, halafu kwenye shughuli yako akutose, jamani lazima ungejisikia vibaya. Yule mtoto inaonekana hana washauri wazuri.”
AHADI ZAKE
“Kwanza Lulu hakutokea kwenye kikao cha kwanza, alikuja kwenye kikao cha pili. Aliahidi kuwa suala la mapambo angeshughulikia yeye, pia angetoa gari aina ya Vogue kwa ajili ya kumbeba Muna na wapambe wake halafu pia akasema angetoa shilingi milioni moja.
“Watu tulifurahi sana, tukawa na uhakika kuwa mambo hayo tusihangaike nayo kabisa kwa kuwa yeye angeyatimiza. Hatukuwa na shaka naye kwa sababu tunajua walipotoka na Muna.”
ATEULIWA MWENYEKITI
“Unaona sasa! Kutokana na ahadi zake, watu wakaona kwa nini wasimpe heshima ya uenyekiti ili asimamie kila kitu? Mmoja akatoa hilo wazo, wote tukaliunga mkono, naye akaridhia kuwa angekuwa mwenyekiti, lakini cha ajabu akawa anakacha vikao, kila siku akawa mtu wa visingizio.”
KUTOKA VOGUE, MAPAMBO, TSH. 1,000,000 MPAKA TSH. 200,000
“Baada ya chenga nyingi sana, hatimaye alikuja kutuma shilingi laki mbili tu, basi. Hebu fikiria kutokea kwenye gari, mapambo na milioni moja anakuja kutoa laki mbili tu.
“Hilo jambo kwa kweli limemkasirisha sana Muna. Unajua Muna anadai wakati akiwa jela mpaka anatoka, alitumia zaidi ya milioni 10, sasa alichokiahidi kilikuwa ni kitu kizuri cha kiungwana kwa ajili ya kuendeleza umoja, lakini mwenzake amekuja kumuangusha.
“Ni afadhali angetoa udhuru au angesema kuwa kuna matatizo, yeye alikuwa anamkimbia mwenzake na mbaya zaidi kuna wakati alikuwa akimzimia simu kabisa.”
AKACHA SHEREHE
“Kilichomuuma zaidi Muna ni kitendo cha kukacha hata sherehe yenyewe. Mastaa kibao walikuja lakini yeye hakukanyaga. Hali siyo shwari kabisa we’ ingia hata kwenye Instagram ya Muna (ukurasa wake) kuna vitu kaviandika utagundua tu anamaanisha nini kati yake na Lulu.”
GONGA HAPA KUMSIKIA MUNA
Siyo desturi ya Risasi Mchanganyiko kutoa habari bila kutoa nafasi kwa wahusika wajieleze. Kwa kuzingatia hilo, mapaparazi wetu walimsaka Muna ambaye alitoa ushirikiano wa kutosha.
“Ni kweli nina tofauti na Lulu kwa sasa, hayo unayoeleza yote yametokea. Ni kweli kabisa lakini kwa sasa sipo tayari kuzungumzia kwa undani kuhusiana na ishu hiyo.
“Hayo mambo kama ni kupita yameshapita, sasa hivi naangalia mambo mengine. Tuachane na hayo kaka yangu,” alisema Muna.
Alipobanwa afafanue japo kiduchu, alisema: “Lulu kweli amenikosea sana na sikutegemea kama angekuja kunifanyia vitu kama vile.
“Yaani kama nisingekuwa na watu wa kunisaidia na kunisimamia sijui ningeificha wapi aibu iliyotaka kutokea! Kwa kweli sijui ningekuwa mgeni wa nani, lakini tuyaache tu, yamepita.”
HUYU HAPA LULU
Lulu naye alipatikana na kuzungumzia ishu hiyo ambapo alisema: “Ni kweli sikwenda katika shughuli ya Muna, najua mwenyewe nini kilinifanya nisitokee. Muna ana haki ya kulalamika kutokana na hilo lakini mambo yaliingiliana.”
Kuhusu michango alisema: “Mchango wangu mimi nimetoa wote. Vogue kuna mtu aliahidi, siyo mimi.”
Hata hivyo hakutaka kufafanua zaidi kuhusu mapambo na fedha alizotoa kama mchango wake, lakini alisisitiza mchango wake wote alioahidi alikamilisha.